26 Julai 2025 - 23:56
Hospitali ya Ebrahim Hajji Charitable Healthcare Yatangaza Upimaji Bure wa Saratani Kwa Wananchi - Dkt. Molloo Aeleza Mpango Kabambe

“Upimaji wa Saratani tofauti kama ya shingo ya kizazi, matiti, na tezi dume kwa wanaume utafanyika bure kabisa. Wengine watapata matibabu hapo hapo na wale wanaohitaji huduma maalum zaidi watapewa rufaa,” alisema Dkt. Molloo.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- kupitia kipindi cha Uislamu na Jamii - IBN TV Africa imefanya mahojiano na Dkt. Alihussein Molloo, Meneja Utawala - Hospitali ya Ebrahim Hajji (Charitable Healthcare) ambapo ametangaza huduma ya upimaji bure wa aina mbalimbali za Saratani kwa Wananchi wote, na kupatiwa matibabu ya papo kwa hapo.

Katika juhudi za kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa saratani nchini, Hospitali ya Ebrahim Hajji Charitable Healthcare imetangaza mpango maalumu wa upimaji bure wa aina mbalimbali za saratani kwa wananchi wote, ukihusisha:

1_ Saratani ya shingo ya kizazi kwa Wanawake.

2_ Saratani ya matiti.

3_ Saratani ya tezi dume kwa Wanaume.

Akizungumza katika kipindi maalumu cha Uislamu na Jamii kilichorushwa Julai 26, 2025 kupitia IBN TV Africa, Dkt. Alihussein Molloo alieleza kuwa mpango huo unahusisha wataalamu wa afya waliobobea, ambapo baadhi ya wagonjwa watapewa matibabu papo hapo, huku wengine wakipewa rufaa kwa matibabu ya kina zaidi.

Upimaji wa Saratani tofauti kama ya shingo ya kizazi, matiti, na tezi dume kwa wanaume utafanyika bure kabisa. Wengine watapata matibabu hapo hapo na wale wanaohitaji huduma maalum zaidi watapewa rufaa,” alisema Dkt. Molloo.

Mpango huu ni sehemu ya jitihada za Hospitali ya Ebrahim Hajji katika kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora za afya, hasa wale wanaokabiliwa na magonjwa hatari kama Saratani, lakini wanakosa uwezo wa kifedha kufanyiwa vipimo au kupata tiba kwa wakati.

Malengo ni:

1_ Kuongeza uhamasishaji juu ya kuepuka ugonjwa huu wa Saratani.

2_ Kugundua mapema visa vya Saratani ili kurahisisha matibabu.

3_ Kutoa huduma za afya kwa jamii kwa misingi ya huruma na utu.

Hivyo, Wananchi wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hii ya kipekee, kwani utambuzi wa mapema wa saratani unaweza kuokoa maisha. Hospitali hiyo imesisitiza kuwa mpango huu utakuwa wa kuendelea, na utaambatana na kampeni za elimu ya afya katika jamii.

Hospitali ya Ebrahim Hajji Charitable Healthcare Yatangaza Upimaji Bure wa Saratani Kwa Wananchi - Dkt. Molloo Aeleza Mpango Kabambe

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha